2 Desemba 2019 - 07:20
Bunge la Afghanistan lamtaka Rais Ashraf Ghani awaombe radhi wananchi kwa kukutana na Trump

Bunge la Afghanistan sambamba na kumkosoa vikali Rais Ashraf Ghani wa nchi hiyo kutokana na hatua yake ya kukutana na Rais Donald Trump wa Marekani katika kambi ya kijeshi ya Bagram, limemtaka rais huyo awaombe radhi watu wa nchi hiyo.

(ABNA24.com) Wabunge wa Afghanistan wamesema kwamba mkutano wa Trump na Ashraf Ghani katika kambi hiyo, umeibua hasira kubwa ya raia wa nchi hiyo. Katika kikao cha bunge, wabunge kadhaa wametangaza kuwa kitendo cha rais huyo kufika katika kambi ya kijeshi ya Bagram, ambayo ndio kambi kubwa zaidi ya askari wa Marekani nchini Afghanistan, kiliuweka chini ya swali kujitawala kwa Afghanistan kama ambavyo pia  kiliwavunjia heshima raia wa taifa hilo.

Itakumbukwa kuwa Alkhamisi ya tarehe 28 Novemba Trump alifanya safari ya kinyemela na ya kushtukiza ya kuwatembelea askari wa nchi yake waliopo kwenye kambi ya kijeshi ya Bagram kama ambavyo pia alikutana na Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan pamoja na Asadullah Khalid, Kaimu Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo.

Safari ya rais huyo wa Marekani nchini Afghanistan na kitendo cha Rais Ashraf Ghani kwenda kumuona katika kambi hiyo, kimekosolewa sana na raia, vyombo vya habari, wanasiasa na weledi mashuhuri wa masuala ya kisiasa wa nchi hiyo.

Sisitizo la wabunge linalomtaka rais huyo kuwaomba radhi wananchi kutokana na hatua yake ya kuuvunjia heshima kujitawala kwa Afghanistan katika safari ya kinyemela ya Trump kwenye kambi ya kijeshi ya Bagram, linaakisi hasira za wananchi na wabunge wa nchi hiyo kutokana na kudhalilishwa na rais huyo wa Marekani.

Kuhusiana na suala hilo, Abdulkarim Khoram, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan anasema: "Yale yaliyojiri wakati wa safari ya Rais Donald Trump wa Marekani katika kambi ya kijeshi ya Bagram, yalikuwa kinyume cha demokrasia na taratibu zote za kidiplomasia." Hii ni kusema kuwa, raia na shakhsia wa kisiasa, viongozi wa vyama vya siasa na wanaharakati wa vyombo vya habari nchini Afghanistan walitaraji kwamba Rais Ashraf Ghani asingeenda kukutana na Trump kwa kuwa aliingia kinyemela katika nchi hiyo, na hivyo kukosoa tabia hiyo isiyo sahihi ya Trump kama ambavyo pia angekuwa amelinda heshima na hadhi ya nchi hiyo ya Asia.

Kuhusiana na suala hilo Ahmad Saidi, mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa wa mjini Kabul, mji mkuu wa Afghanistan anasema: "Kitendo cha Rais Ashraf Ghani ambaye ni mwakilishi wa nchi huru inayojitawala kwenda kwenye kambi ya Bagram ya askari wa Marekani kwa ajili ya kukutana na Trump na miamala yake, yote hayo hayakuwa sahihi kabisa.

" Mbali na kwamba raia na shakhsia tofauti wa Afghanistan wanasisitizia kwamba rais wa nchi hiyo hakupaswa kwenda kukutana na Trump katika kambi ya Bagram, bali walitakiwa kukutana katika ikulu ya rais wa nchi hiyo mjini Kabul. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, baada ya kumalizika hotuba ya Rais Ashraf Ghani katika kambi ya kijeshi ya Bagram, Trump aliwataka askari wa Marekani kumfungulia njia rais huyo na kuondoka huku akimuacha hapo rais huyo wa Marekani, jambo ambalo limekosolewa vikali na raia wa nchi hiyo kupitia mitandao ya kijamii.

Abdul Latif Pedram, mwanaharakati wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan ambaye pia ni mgombea wa urais amesema: "Trump alimdhalilisha Ashraf Ghani kwa makusudi, mtu ambaye anadai kuwa kiongozi wa nchi  sambamba na kuionyesha dunia kwamba hawathamini hata kidogo viongozi wa serikali ya Afghanistan.

" Ni katika mazingira hayo ndio maana wabunge wa Afghanistan wakatoa radiamali kali kutokana na kitendo cha rais wa nchi hiyo kukutana katika kambi ya kijeshi ya Bagram na Rais Donald Trump aliyefanya safari ya kinyemela na ya kificho ndani ya taifa hilo.

Mbali na radiamali hiyo, wamemtaka pia Rais Ashraf Ghani kuwaomba msamaha wananchi wa Afghanistan ili kupunguza hasira yao iliyotokana na rais huyo kuivunjia heshima nchi yao.

........
340